MTAKATIFU MARCELLINUS NA PETRO, WASHUHUDA
Tuna deni gani kwa Mungu na wajibu wetu kwa wengine ni upi?
Mtume Paulo anatuambia kwamba ni lazima tumpe kila mmoja kile anachostahili (Warumi 13:6–8).
Viongozi wa Kiyahudi walijaribu kumnasa Yesu katika mgogoro wa kidini na kisiasa kuhusu suala la kodi. Wayahudi walichukia watawala wa kigeni na walichukia pia kulipa kodi kwa Kaisari. Kwa hiyo walimwekea Yesu swali gumu ili kumjaribu, wakitaka aseme jambo wanaloweza kulitumia dhidi yake.
Kama Yesu angesema ni halali kulipa kodi kwa mtawala wa kipagani, angepoteza uaminifu mbele ya Wayahudi, ambao wangemwona kama mwoga na rafiki wa Kaisari. Lakini kama angesema si halali kulipa kodi, Mafarisayo wangekuwa na sababu ya kumpeleka kwa Warumi na kumshutumu kama mchochezi wa kisiasa ili akamatwe.
Yesu aliepuka mtego wao kwa kutumia mfano wa sarafu. Katika ulimwengu wa kale, sarafu zilikuwa na nguvu kubwa ya kisiasa. Watawala walikuwa wakichonga sura na jina lao kwenye sarafu, na kwa namna fulani sarafu ilionekana kuwa mali ya mfalme. Pale sarafu ilipotumika, ilionyesha mamlaka ya mtawala husika.
Kwa kuwa Wayahudi walitumia fedha ya Kirumi, Yesu alieleza kwamba kile kilicho cha Kaisari kimpelekwe Kaisari.
Injili ya Yesu kuhusu Kaisari na Mungu inapata uhai katika ushuhuda wa Watakatifu Marcellinus na Petro, ambao walithibitisha kwa maisha yao kwamba mamlaka ya dunia ina mipaka yake, lakini Mungu hana mipaka katika utii wa mwanadamu. Walimpa Kaisari kile kilichokuwa cha Kaisari kwa heshima, lakini hawakukubali kumpa Kaisari kile kilicho cha Mungu—yaani imani yao. Kwa kifo chao cha kishahidi, walionesha ukweli kwamba mwanadamu ameumbwa kwa sura ya Mungu, hivyo maisha yake, moyo wake na uaminifu wake haviwezi kuuzwa kwa mamlaka ya dunia. Hivyo, ujumbe wao unasisitiza kwamba uaminifu kwa Mungu ni wa milele, hata pale ambapo dunia inadai gharama kubwa.
Pd. Benjamin Maganga Bundala