Skip to Content

KUMBUKUMBU YA WAT. MASHAHIDI WA UGANDA

Wat. Karoli Lwanga na wenzake, mashahidi.

KUMBUKUMBU YA WAT. MASHAHIDI WA UGANDA

Leo, pamoja na Kanisa lote tunawaheshimu Mashahidi wa Uganda: Ni Waafrika 22 ambao waliteswa kati ya mwaka 1885 na 1887 wakati mdhalimu Mwanga alipokuwa Kabaka. yaani Mfalme, wa Uganda. Wao ni mashahidi wa kwanza wa Afrika Kusini mwa Sahara. Ni kikundi cha matarishi wa kifalme waliokuwa Wakatoliki na Waanglikana. Baadhi yao walikuwa wakatekumeni bado. Kwa uovu wake Mwanga aliwashurutisha wakristo watende maovu, walipokataz akaanza kuwatesa vikali. Mukajanga alıkuwa ndiye kiongozi wa wauaji. Matias Mulumba alikatwa mikono na miguu na kuchunwa ngozi ya kifuani na mgongoni akafa katika mateso makali.

Karoli Lwanga na wenzake 12, ambao ni Kizito, Mbaga Tuzinde, Bruno Serunkuma, Jakobo Buzabaliawo, Ambrozi Kibuka, Mugaga, Gyavira, Achile Kiwanuka Adolfu Ludigo, Mukasa, Anatoli Kirigwajo, Atanaz Bazekuketa, Gonzaga Gonza, na Luka Banabakintu walichomwa moto tarehe 3 Juni, 1886. Hilo lilitendeka Namugongo, nje ya Kampala. Yosefu Mukasa naye alichomwa moto; Andrea Kagwa alikatwa kichwa; Dionz Sebugwao, Ponsiano Ngondwe na Noe Mawagali walichomwa mkuki, Joani Muzeyi alitupwa ziwani akafa Tarehe 18 Oktoba, 1964, Baba Mt. Paulo VI akawatangaza kuwa Watakatifu.

Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake mashahidi wa Uganda ni mfano wa watu waliobaki waaminifu kwa Kristo hata katikati ya mateso, vitisho na kifo. Walikumbuka maneno ya Yesu: “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu, lakini mwenye kuvumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka.” Nao hawakurudi nyuma wala kuacha imani yao, bali walivumilia mpaka mwisho wakiamini kuwa utukufu wa Mungu ni mkuu kuliko mateso ya dunia.

Nasi leo tunapokutana na dharau, majaribu, kukataliwa au changamoto kwa sababu ya kufanya yaliyo mema na kumfuata Kristo, tunaitwa kuwa na moyo huo huo wa uvumilivu. Ujumbe wao unatukumbusha kwamba ushindi wa Mkristo haupatikani kwa kuishi bila matatizo, bali kwa kusimama imara katika imani hadi mwisho. Mungu huwapa nguvu wale wanaomtegemea, na thawabu ya uaminifu ni uzima wa milele.