Mpendwa msomaji wangu, habari za leo! Karibu tena katika safari ya tafakuri za maisha. Bila wewe mimi siwezi kuandika. Ninaendelea kukushukuru kwa muda wako wa kusoma tafakuri zangu.
Wiki hii nimeona tusafiri pamoja katika kumtafakari rafiki yangu mmoja anayependa kuanzisha biashara ya duka la nguo ingawa huwa hapendi kero. Ana hamu ya kutoboa kimaisha kupitia biashara ya nguo lakini ninavyomjua, huwa hapendi kabisa kero na kusumbuana na watu.
Kwanza, nilivyomsikiliza na nikawaza alivyo, nikasema kazi anayo. Hivi sisi wateja anatujua vizuri au anatusikia! Wiki hii nimeamua niandike makala kwa ajili yake ili ajitafakari kama muziki anauweza. Ngoja nimweleze sisi wateja tulivyo sasa:
1. Tupo tunaouliza na kulinganisha kisha tunapotea au kukurudia. Wenye biashara ni wengi. Kwa hiyo, sisi wateja wakati mwingine tuna maringo. Tunaweza kuja kwako tukacheki kama vile kweli tunanunua kisha tunakwenda sehemu nyingine ili kulinganisha bei na ubora. Tukiona bidhaa zako bado ni nzuri na bei ni zile tunazotaka, basi tunakurudia. Je, uko tayari tukirudi utuhudumie bila kuanza kutuzodoa eti kwa nini tumerudi! Utaweza kukaa kimya wewe! Na ukituudhi tu, tunajiondokea. Sisi ndio wateja bwana!
2. Tupo ambao tunakaguakagua bidhaa zako kwa kushikashika na kuacha. Bila kujali utasemaje, wengine tutagusagusa weee, kisha tunaondoka bila hata kuuliza bei. Ole wako utuseme, siku nyingine tukija tutakuwa tunakuruka bila hata kukutazama. Sisi ndio sisi. Wafanyabiashara mko wengi. Utuudhi uone. Shauri yako!
3. Tupo ambao tunazodoa na kunanga biashara yako ili tu utupunguzie bei. Kwa kuwa mko wengi, wakati mwingine huwa tunazipa kasoro bidhaa zako ili tupate fursa ya kupunguziwa bei. Sasa wewe jifanye unakasirika uone! Tunaondoka zetu bila hata kuuliza bei. Sisi ndio wateja na lazima uendane na sisi. Kama hutaki acha biashara.
4. Wengine wetu tunakuja kwenye biashara yako kuzugazuga tu ili muda uende. Kuna wakati tunachoka kukaa sehemu moja. Kwa hiyo, siku nyingine huwa tunajisikia kwenda Mlimani City au Kariakoo kupoteza tu muda. Kama kwako kuna benchi, nikichoka ninakaa ili nipumzike. Nikiona unanikazia macho najiulizisha bei ya bidhaa zako ili utulie. Sisi wateja tuna raha sana. Wewe ukionesha una hasira, siku nyingine hatuji sasa!
5. Wale wetu wanaotembelea biashara yako ili tu kutembea na kupoteza muda. Wakati mwingine tunachoka kukaa mahali pamoja. Hivyo, katika siku fulani, tunajisikia tu kwenda Mlimani City au Kariakoo kupoteza muda. Ikiwa una benchi katika duka lako, nitakaa kupumzika nitakapochoka. Ikiwa nitakugundua unaniangalia kwa shaka, nitauliza kwa kawaida kuhusu bei ya vitu vyako ili kukutuliza. Sisi wateja tuna maisha mazuri! Ikiwa utaonyesha kuwa unakasirika, sawa, hatutarudi tena wakati ujao!
Mpendwa msomaji wangu, unatuonaje sisi wateja! Uko tayari kufanya biashara na sisi! Yaani, kwa sasa ukija na stress zako kwenye biashara, utajiuzia mwenyewe. Sisi tuna maringo kama yote. Tunaamua tununue leo au siku nyingine. Ole wako utuseme! Hii ndiyo raha ya biashara huria katika ulimwengu wa kibepari. Yaani, wewe muuzaji nawe ni bidhaa. Ukijisahau ukaanza kutufokea, hatukununulii vitu vyako. Tunazira na kuondoka. Lazima utubembeleze.
Mpendwa msomaji wangu, tafakauri ya wiki hii imetumia mfano wa rafiki yangu kama sehemu tu ya kuanzia. Unaweza kupanua tafakuri hii kwa kuangalia nyanja tofauti na biashara.
Msisitizo wa tafakuri hii ni kwamba hakuna kazi inayohusicha watu isiyo na kero. Mradi wowote unaowaza kuupanga, umejiandaa kukabiliana na kero au changamoto! Uko tayari kuepuka kutoa lugha mbaya na kutubembeleza! Ukitusema tu, sisi haoooooooo!
Ninakutakia wiki njema. Tuonane tena Jumatatu ijayo. Asante sana kwa kusoma tafakuri yangu
=================
©️ Leonard Bakize, 2026
Juni 8, 2026
+255 755 643 590
eternalword2018@gmail.com
Ninakutakia wiki njema. Tuonane tena Jumatatu ijayo. Asante sana kwa kusoma tafakuri yangu.