Skip to Content

KALAMU YANGU, RAI YANGU!

Ikiwa wewe ni Kuku wa "Broiler", Amka, Ni Alfajiri
7 Juni 2026 na
DR. LEONARD BAKIZE

Kama Wewe ni Kuku wa KIZUNGU, amka Kumekucha!

Mpendwa msomaji wangu, unaendeleaje? Mimi sijambo kabisa. Niko tayari kusafiri nawe katika ulimwengu wetu wa tafakuri. Funga mkanda twende zetu sasa.

Ninaomba nianze kwa kukuuliza kwanza. Wewe ni kuku wa Kizungu au Kienyeji? Usinijibu sasa hivi. Tuendelee na safari kisha utanitumia jibu lako baadaye.

Wakati nikitafakari kuhusu nini cha kukuandikia wiki hii, nimejikuta sina cha maana sana. Hata hivyo, hebu tupige tu stori kadhaa za kirafiki ili tutafakari kwa namna hii. Kuna mambo kadhaa nimeyakumbuka nikasema nikushirikishe huenda nawe unayakumbuka, na kupitia hayo, tutapata tafakuri.

Mosi, wakati fulani nikiwa shule ya msingi, tulikuwa tunapenda kutaniana sana darasani. Kuna wasichana walikuwa wanapenda kututania sisi wavulana. Siku moja msichana mmoja alitutania akisema ninawaonea huruma nyie wavulana. Pambaneni mfaulu. Akasema, mie kuna mtu anasota huko kwa ajili yangu. Kwa hiyo msiniige eti!"

Nimekumbuka ushauri huo wa baadhi ya akina dada nikajikuta ninawaza, Hivi leo kuna anayewaza tena hivyo kweli! Huenda kwa kipindi kile ilikuwa sawa, lakini kwa leo mhuu hatari!

Pili, kabla sijapumzika nikakumbuka jamaa yangu mmoja tukiwa sekondari katika shule fulani. Sisi tukiwa tunafanya mijadala na kujisomea usiku, yeye alikuwa anatucheka. Ukimuuliza unacheka nini alikuwa anasema, Ninawaonea huruma mnavyosota. Mimi akhaaa! Uncle yuko kwenye mfumo. Nikimaliza tu, lazima afanye kitu. Mtakuja kunielewa baadaye. Lakini sasa hiyo baadaye ilipofika, mhuuu hata sijui nini kilitokea upepo ukaenda ndivyo sivyo.

Tatu, kulikuwa na fikra kwamba baba/mama/uncle yupo, lazima atafanya mambo. Hawezi kukubali nipotee. Mpendwa msomaji wangu, katika safari yangu na pengine yako, wapo wengi ambao wamepuuzia kusoma au kufanya juhudi binafsi kwa kisingizio kwamba mzazi au ndugu yupo. Eti kwa jinsi mzazi/mlezi au ndugu anavyowapenda, hawezi kukubali wapotee. Wewe hujawahi kukutana na watu wenye fikra hizo kweli? Basi utanijibu baadaye. Tuendelee na safari.

Nne, kulikuwa na imani ya mambo yatajipa yenyewe. Nimewahi kukutana na watu ambao hawataki kuteseka leo kwa mtazamo wa kuwa na kesho nzuri. Wao mara zote huwakejeli wanaopambana kwa kusema kwamba unaweza kuteseka sana leo ukajikuta hiyo kesho huioni. Hawa wanaganga ya leo tu, yajayo yatajipa yenyewe. Sijui huu tuuite uzembe au uvivu! Au basi!

Mpendwa msomaji wangu, mifano hiyo imenifanya niutafakari ulimwengu wa sasa na kujikuta ninamuonea huruma mtu ambaye bado ana mawazo hayo ya kufanyiwa mambo. Ama kweli, kila zama na mambo yake! Leo hii ni kila mbuzi kula kulingana na urefu wa kamba yake. Wewe ukijisahau ukabaki na kamba fupi, utajikuta unakula mpaka udongo baada ya nyasi zako chache kuisha. Lazima upambane kuhakikisha kamba yako inarefuka ili ule vizuri na kuwa na nyasi mpya kila siku.

Katika ulimwengu wa kibepari, kila mtu amekuwa bidhaa. Ndiyo, na wewe hapo ni bidhaa! Ukizubaa, utaozea sokoni. Shauri yako! Leo hii, kila mmoja yuko katika soko ambalo linamlazimisha kuwa mbunifu sana, mwanafunzi wa kujifunza kila kinachotokea, mtafutaji wa fursa mpya, mpambanaji katika kupenya kwenye msongamano, n.k. Ukibaki kama kuku wa Kizungu, utadhalilika, utawaonea watu wivu bila sababu, utateseka na mwisho utakufa haraka kibiashara.

Ninapotumia mfano wa kuku wa Kizungu, wala sina lengo la kumtukana mtu. Nimejikuta tu ninapata mfano wa aina hiyo ya kuku nikaona si vibaya tukijifunza kwao. Kuku huyo wa Kizungu, ni zezeta. Wakati mwingine, hata milango ikifunguliwa atoke, yeye hajui. Mpaka mwenye kuku aje na kupiga kengele ya kula au kufanya lolote. Ndugu yangu, tuko katika ulimwengu wa kuamka na kuwa kuku wa kienyeji.

Leo hii, wajanja, hata kama wana wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kwenye mifumo, wanapambana kama vile hawana yeyote wa kumtegemea. Wewe ukibaki kuwa kuku wa Kizungu, shauri yako! Maisha haya hayaeleweki. Mzazi au mtegemezi anaweza kutoweka muda wowote usioutarajia. Ukiwa na wa kukusaidia, basi akusaidie kukuongezea tu nguvu. Usiwe kuku wa Kizungu anayesubiri connection au maelekezo ya mwenye kuku. Usisubiri kuamshwa unywe maji, ule, uamke, utembee, n.k.

  • Kama uko shule, ninadhani ushanielewa ninachotaka ufanye. Pambana kama vile huna wazazi au ndugu. Ipo siku utanishukuru.

  • Kama ulipewa connection mpaka ukafika hapo ulipo, basi fanya kazi mpaka watu waone uwezo wako na jisimamie wewe kama wewe kama vile hakuna connection. Usikubali tena kuwa kuku wa Kizungu.

  • Kama biashara zako zinategemezwa na mtu, leo elewa kwamba mtu au watu hao watatoweka. Pambana mpaka ujisimamie. Komaa ili uwe kuku wa kienyeji asiyelala njaa eti kwa sababu ya mvua, joto, baridi, umande, ukungu, mwewe, wala kimburu.

Sikuambii ukatae msaada wa mtu bali ninakukumbusha tu kwamba huyo mtu au ndugu siyo jiwe. Muda wowote watu hao wanaweza kupotea. Usiponielewa, wategemezi wako wakipotea ukabaki mwenyewe, utaona kama vile umefikia mwisho wa maisha yako, kumbe si kweli.

Mpendwa msomaji wangu, tusikubali kuwa kuku wa Kizungu. Maisha yamebadilika sana. Kama nimekukwaza mahali kwa mifano yangu, nisamehe. Lakini kamwe usikubali kuwa kuku wa Kizungu.

Asante sana kwa kusoma makala yangu. Uwe na Jumatatu njema. Tukutane tena Jumatatu ijayo. Hivi nikikuomba unifadhili ili makala hizi zizae kitabu, unaweza! Njoo uninong'oneze huku kikashani (inbox).

©️ Leonard Bakize, 2026

Mei 25, 2026

+255 755 643 590

eternalword2018@gmail.com

KALAMU YANGU, RAI YANGU!
Hakika, Unataka Kufanya Biashara, lakini Je, Unaweza Kustahimili Wateja Hawa?